
« Kwa kweli, pia kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa kirefu, nadhani ulimwengu haungekuwa na nafasi ya kuviweka vitabu vya kukunjwa ambavyo vingeandikwa » (Yohana 21:25)
Yesu Kristo na muujiza wa kwanza ulioandikwa katika Injili ya Yohana, anageuza maji kuwa divai: « Basi siku ya tatu kulikuwa na karamu ya ndoa katika Kana ya Galilaya, na mama ya Yesu alikuwa huko. Yesu na wanafunzi wake pia walikuwa wamealikwa kwenye karamu hiyo ya ndoa. Divai ilipopungua mama ya Yesu akamwambia: “Hawana divai.” Lakini Yesu akamjibu: “Mwanamke, jambo hilo linatuhusuje mimi na wewe? Bado saa yangu haijafika.” Mama yake akawaambia wahudumu: “Fanyeni lolote atakalowaambia.” Kulikuwa na mitungi sita ya maji hapo kulingana na sheria za utakaso za Wayahudi, kila mmoja ulikuwa na uwezo wa kuchukua vipimo viwili au vitatu vya maji. Yesu akawaambia: “Ijazeni mitungi hiyo maji.” Nao wakaijaza pomoni. Akawaambia: “Choteni kidogo na kumpelekea msimamizi wa karamu.” Basi wakampelekea. Msimamizi wa karamu alipoonja maji yaliyokuwa yamegeuzwa kuwa divai, bila kujua divai ilitoka wapi (lakini wahudumu waliokuwa wamechota maji hayo walijua), akamwita bwana harusi akamwambia: “Kila mtu hutoa divai nzuri kwanza, kisha hutoa divai hafifu wakati ambapo watu wameingiwa na kileo. Lakini wewe umehifadhi divai nzuri mpaka sasa.” Yesu alifanya muujiza huo wake wa kwanza katika Kana ya Galilaya, kwa hiyo akaonyesha utukufu wake, na wanafunzi wake wakamwamini » (Yohana 2:1-11).
Yesu Kristo anamponya mwana wa mtumishi wa mfalme: « Kisha Yesu akaja tena Kana ya Galilaya, ambako alikuwa amegeuza maji kuwa divai. Basi kulikuwa na ofisa fulani wa mfalme ambaye mwana wake alikuwa mgonjwa huko Kapernaumu. Mtu huyu aliposikia kwamba Yesu ametoka Yudea na kuja Galilaya, akamwendea na kumwomba ashuke kwenda kumponya mwanawe, kwa maana alikuwa karibu kufa. Lakini, Yesu akamwambia: “Msipoona ishara na maajabu, hamtaamini kamwe.” Yule ofisa wa mfalme akamwambia: “Bwana, twende kabla mwanangu hajafa.” Yesu akamwambia: “Rudi nyumbani; mwanao yuko hai.” Yule mtu akaamini maneno ambayo Yesu alimwambia, akaondoka. Lakini akiwa njiani akakutana na watumwa wake, wakamwambia kwamba mwanawe yuko hai. Kwa hiyo akawauliza saa ambayo alipata nafuu. Wakamjibu: “Alipona homa jana saa saba.” Kwa hiyo yule baba akajua ilikuwa saa ileile ambayo Yesu alimwambia: “Mwanao yuko hai.” Basi yeye na watu wote wa nyumbani kwake wakaamini. Huo ulikuwa muujiza wa pili ambao Yesu alifanya alipotoka Yudea na kwenda Galilaya » (Yohana 4:46-54).
Yesu Kristo anamponya mtu mwenye pepo katika Kapernaumu: « Kisha akashuka kwenda jiji la Kapernaumu, huko Galilaya. Naye alikuwa akiwafundisha siku ya Sabato, nao wakashangazwa na njia yake ya kufundisha, kwa sababu alikuwa akizungumza kwa mamlaka. Basi katika sinagogi kulikuwa na mtu mwenye roho mwovu, naye akapiga kelele akisema: “Ah! Kwa nini unatusumbua, wewe Yesu Mnazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Ninajua wewe ni nani, Mtakatifu wa Mungu.” Lakini Yesu akamkemea, akisema: “Nyamaza na umtoke.” Basi baada ya kumwangusha mtu huyo mbele yao, yule roho mwovu akamtoka bila kumuumiza. Wote wakashangaa na kuanza kuambiana: “Anazungumza kwa mamlaka sana! Anawaagiza roho waovu kwa mamlaka na nguvu, nao wanatoka!” Basi habari kumhusu zikazidi kuenea kila mahali katika maeneo yaliyokuwa karibu » (Luka 4:31-37).
Yesu Kristo anafukuza pepo katika nchi ya Wagerasi (sehemu ya mashariki ya Yordani, karibu na Ziwa Tiberia): « Alipofika upande ule mwingine na kuingia katika eneo la Wagadarene, alikutana na wanaume wawili waliokuwa na roho waovu wakitoka makaburini. Walikuwa wakali sana, hivi kwamba hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kupita katika barabara hiyo. Na tazama! wakapiga mayowe wakisema: “Kwa nini unatusumbua, Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati uliowekwa?” Lakini kule mbali nao kulikuwa na kundi la nguruwe wengi wakila. Kwa hiyo wale roho waovu wakaanza kumsihi: “Ukitufukuza, turuhusu tuingie katika lile kundi la nguruwe.” Basi akawaambia: “Nendeni!” Ndipo wakatoka na kuingia ndani ya wale nguruwe, na tazama! kundi zima likatimua mbio, likaruka poromoko likazama baharini na kufa maji. Lakini wachungaji wakakimbia, na walipoingia jijini, wakasimulia mambo yote, kutia ndani habari kuhusu wale watu waliokuwa na roho waovu. Na tazama! watu wote katika jiji hilo wakaenda kukutana na Yesu, na walipomwona, wakamsihi aondoke katika eneo lao » (Mathayo 8:28-34).
Yesu Kristo alimponya mama mkwe wa mtume Petro: « Yesu alipoingia nyumbani kwa Petro, alimwona mama mkwe wa Petro akiwa amelala akiugua homa. Basi Yesu akamgusa mkono, naye akapona homa, akasimama na kuanza kumhudumia » (Mathayo 8:14,15).
Yesu Kristo anamponya mtu aliyepooza mkono: « Siku nyingine ya Sabato aliingia katika sinagogi, akaanza kufundisha. Kulikuwa na mtu aliyepooza mkono wa kulia. Waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimwangalia Yesu kwa makini ili waone kama angeponya katika siku ya Sabato, ili wapate sababu ya kumshtaki. Hata hivyo, alijua mawazo yao, basi akamwambia yule mtu aliyepooza mkono: “Inuka usimame hapa katikati.” Naye akainuka na kusimama hapo. Kisha Yesu akawauliza: “Je, ni halali kufanya mema au kufanya mabaya siku ya Sabato, kuokoa uhai au kuuangamiza?” Baada ya kuwatazama wote waliokuwapo, Yesu akamwambia mtu huyo: “Nyoosha mkono wako.” Akaunyoosha, nao ukapona. Lakini wakakasirika sana, wakaanza kushauriana kuhusu jambo ambalo wangemtendea Yesu » (Luka 6:6-11).
Yesu Kristo huponya mtu anayesumbuliwa na ugonjwa wa edema, mkusanyiko mkubwa wa maji katika mwili: « Siku moja ya Sabato, Yesu alienda kula chakula katika nyumba ya kiongozi mmoja wa Mafarisayo, nao walikuwa wakimtazama sana. Tazama! mbele yake kulikuwa na mtu mwenye ugonjwa wa kuvimba mwili. Basi Yesu akawauliza wale wenye ujuzi wa Sheria na Mafarisayo: “Je, ni halali au si halali kumponya mtu siku ya Sabato?” Lakini wakanyamaza. Basi akamshika mtu huyo, akamponya na kumwambia aende zake. Kisha akawauliza: “Ni nani kati yenu ambaye mwana wake au ng’ombe wake akianguka ndani ya kisima siku ya Sabato, hatamtoa humo mara moja?” Wakashindwa kumjibu » (Luka 14:1-6).
Yesu Kristo huponya mtu aliyekuwa kipofu: « Yesu alipokaribia Yeriko kipofu mmoja alikuwa ameketi kando ya barabara akiombaomba. Aliposikia umati ukipita, akaanza kuuliza kilichokuwa kikiendelea. Wakamjibu: “Yesu Mnazareti ndiye anayepita!” Ndipo akasema kwa sauti kubwa: “Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!” Wale waliokuwa mbele wakaanza kumkemea wakimwambia anyamaze, lakini akazidi kusema kwa sauti kubwa: “Mwana wa Daudi, nihurumie!” Kisha Yesu akasimama na kuagiza mtu huyo aletwe kwake. Alipokaribia, Yesu akamuuliza: “Unataka nikufanyie nini?” Akasema: “Bwana, naomba niweze kuona tena.” Basi Yesu akamwambia: “Ona tena; imani yako imekuponya.” Mara moja akaanza kuona tena, naye akaanza kumfuata Yesu huku akimtukuza Mungu. Pia, watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu » (Luka 18:35-43).
Yesu Kristo anaponya vipofu wawili: « Yesu alipokuwa akitoka huko, wanaume wawili vipofu wakamfuata, wakipaza sauti: “Tuhurumie, Mwana wa Daudi.” Alipoingia ndani ya nyumba, wale wanaume vipofu wakamjia, Yesu akawauliza: “Je, mna imani kwamba ninaweza kufanya hivyo?” Wakamjibu: “Ndiyo Bwana.” Kisha akayagusa macho yao, akasema: “Na itendeke kwenu kulingana na imani yenu.” Na macho yao yakaanza kuona. Zaidi ya hayo, Yesu akawaonya vikali: “Msimwambie yeyote jambo hili.” Lakini walipotoka nje, wakaeneza habari kumhusu katika eneo hilo lote » (Mathayo 9:27-31).
Yesu Kristo anaponya bubu kiziwi: « Yesu aliporudi kutoka eneo la Tiro akapitia Sidoni, Dekapoli, na kufika Bahari ya Galilaya. Basi wakamletea mtu aliye kiziwi na mwenye tatizo la kuzungumza, nao wakamsihi aweke mkono juu yake. Kisha akampeleka faraghani, mbali na umati. Halafu akamtia vidole masikioni, baada ya kutema mate, akamgusa ulimi. Yesu akatazama mbinguni, akavuta pumzi kwa nguvu na kumwambia: “Efatha,” yaani, “Funguka.” Ndipo masikio yake yakafunguliwa, na tatizo lake la kuzungumza likaisha, naye akaanza kuzungumza vizuri. Kisha akawaamuru wasimwambie mtu yeyote, lakini kadiri alivyowakataza, ndivyo walivyozidi kutangaza jambo hilo. Kwa kweli, walishangaa sana wakasema: “Amefanya mambo yote vema. Hata anafanya viziwi wasikie na wasio na uwezo wa kusema, wazungumze.” » (Marko 7:31-37).
Yesu Kristo huponya mtu mwenye ukoma: « Mtu fulani mwenye ukoma akamjia, akapiga magoti na kumwomba: “Ikiwa tu unataka, unaweza kunitakasa.” Ndipo akamsikitikia, akanyoosha mkono wake, akamgusa na kumwambia: “Ninataka! Takasika.” Mara moja ule ukoma ukaisha, akawa safi » (Marko 1:40-42).
Uponyaji wa wale kumi wenye ukoma: « Alipokuwa akienda Yerusalemu, alipita kati ya Samaria na Galilaya. Alipokuwa akiingia katika kijiji fulani alikutana na wanaume kumi wenye ukoma, lakini walisimama mbali naye. Kisha wakasema kwa sauti kubwa: “Yesu, Mwalimu, tuhurumie!” Alipowaona, akawaambia: “Nendeni mkajionyeshe kwa makuhani.” Basi walipokuwa wakienda wakatakaswa. Mmoja wao alipoona amepona, akarudi akimtukuza Mungu kwa sauti kubwa. Akaanguka kifudifudi miguuni pa Yesu na kumshukuru. Isitoshe, alikuwa Msamaria. Yesu akauliza: “Wote kumi walitakaswa, sivyo? Basi, wako wapi wale wengine tisa? Je, hakuna mwingine aliyerudi ili kumtukuza Mungu isipokuwa mtu huyu wa taifa lingine?” Kisha akamwambia: “Simama uende; imani yako imekuponya.” » (Luka 17:11-19).
Yesu Kristo huponya mtu aliyepooza: « Baada ya hayo kulikuwa na sherehe ya Wayahudi, na Yesu akapanda kwenda Yerusalemu. Huko Yerusalemu kwenye Lango la Kondoo kulikuwa na dimbwi lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, lenye safu tano za nguzo. Wagonjwa wengi, vipofu, vilema, na wenye viungo vilivyopooza walikuwa wamelala hapo. Lakini hapo palikuwa na mtu fulani aliyekuwa mgonjwa kwa miaka 38. Yesu alipomwona mtu huyo amelala hapo, na akijua kwamba alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu, akamuuliza: “Je, unataka kupona?” Mgonjwa huyo akamjibu: “Bwana, sina mtu wa kuniweka ndani ya dimbwi maji yanapotibuliwa, lakini ninapotaka kuingia, mtu mwingine huingia kabla yangu.”Yesu akamwambia: “Simama! Chukua mkeka wako, utembee.” Mtu huyo akapona mara moja, akabeba mkeka wake na kuanza kutembea” (Yohana 5:1-9).
Yesu Kristo anaponya kifafa: « Walipofika karibu na umati, mtu fulani akamkaribia Yesu, akapiga magoti, na kusema: “Bwana, mhurumie mwanangu, kwa sababu ana kifafa na ni mgonjwa sana. Yeye huanguka ndani ya moto na ndani ya maji mara nyingi. Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini walishindwa kumponya.” Yesu akajibu: “Enyi kizazi kisicho na imani na kilichopotoka, nitaendelea kuwa pamoja nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni hapa.” Kisha Yesu akamkemea yule roho mwovu, naye akamtoka, na yule mvulana akapona kuanzia saa hiyo. Ndipo wanafunzi wakamjia Yesu faraghani na kumuuliza: “Kwa nini tulishindwa kumfukuza?” Akawaambia: “Ni kwa sababu ya imani yenu ndogo. Kwa kweli ninawaambia, mkiwa na imani inayolingana na mbegu ya haradali, mtauambia mlima huu, ‘Ondoka hapa uende pale,’ nao utaondoka, na hakuna jambo litakalowashinda.”” (Mathayo 17:14-20).
Yesu Kristo anafanya muujiza bila kujua: « Yesu alipokuwa akienda umati ukamsonga. Kulikuwa na mwanamke aliyekuwa na mtiririko wa damu kwa miaka 12, na hakuwa amepata mtu wa kumponya. Akaja kutoka nyuma na kugusa upindo wa vazi lake la nje, na mara moja akaacha kutokwa damu. Ndipo Yesu akauliza: “Ni nani aliyenigusa?” Wote walipokuwa wakikana, Petro akasema: “Mwalimu, umati umekuzunguka na kukusonga.” Lakini Yesu akasema: “Mtu fulani amenigusa, kwa maana ninajua nguvu zimenitoka.” Yule mwanamke alipoona kwamba hakuepuka kutambuliwa, akaja akitetemeka na kuanguka chini mbele yake, akaeleza mbele ya watu wote sababu iliyomfanya amguse na jinsi alivyoponywa mara moja. Lakini Yesu akamwambia: “Binti yangu, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.” » (Luka 8:42-48).
Yesu Kristo anaponya kutoka mbali: « Alipomaliza kuzungumza na watu, akaingia Kapernaumu. Ofisa fulani wa jeshi alikuwa na mtumwa aliyempenda sana, na ambaye alikuwa mgonjwa sana karibu kufa. Aliposikia kuhusu Yesu, akawatuma wazee fulani wa Wayahudi wamwombe Yesu aje kumponya mtumwa wake. Walipofika kwa Yesu wakamsihi sana wakisema: “Mfanyie jambo hilo, anastahili kwa maana analipenda taifa letu na yeye ndiye aliyetujengea sinagogi.” Basi Yesu akaenda pamoja nao. Alipokaribia nyumba hiyo, yule ofisa wa jeshi alikuwa tayari amewatuma rafiki zake wamwambie: “Bwana, usijisumbue, kwa maana mimi sistahili uingie ndani ya nyumba yangu. Ndiyo sababu niliona sistahili kuja kwako. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Kwa maana mimi pia niko chini ya mamlaka, na nina wanajeshi walio chini yangu, nami humwambia mmoja, ‘Nenda!’ naye huenda, na mwingine, ‘Njoo!’ naye huja, na mtumwa wangu, ‘Fanya hili!’ naye hulifanya.” Yesu aliposikia maneno hayo alishangazwa naye, akaugeukia umati uliokuwa ukimfuata na kusema: “Ninawaambia, hata katika Israeli sijaona imani kubwa kama hii.” Na wale waliokuwa wametumwa waliporudi nyumbani, wakamkuta yule mtumwa amepona » (Luka 7:1-10).
Yesu Kristo amemponya mwanamke aliyeinama kwa miaka 18: « Sasa Yesu alikuwa akifundisha katika sinagogi siku ya Sabato. Na tazama! hapo palikuwa na mwanamke aliyekuwa na roho ya udhaifu kwa miaka 18, mwili wake ulikuwa umepindika na hangeweza kusimama wima. Yesu alipomwona, akamwambia: “Mwanamke, umefunguliwa kutoka kwa udhaifu wako.” Yesu akaweka mikono juu ya yule mwanamke na mara moja akanyooka na kuanza kumtukuza Mungu. Lakini ofisa msimamizi wa sinagogi akakasirika kwa sababu Yesu aliponya siku ya Sabato, akauambia umati: “Kuna siku sita za kufanya kazi; basi, njooni mponywe katika siku hizo, bali si siku ya Sabato.” Hata hivyo, Bwana akajibu: “Wanafiki, je, kila mmoja wenu hamfungui ng’ombe au punda wake kutoka kwenye kibanda siku ya Sabato na kumpeleka akanywe maji? Je, haifai kwa mwanamke huyu, binti ya Abrahamu, ambaye Shetani alikuwa amemfunga kwa miaka 18 afunguliwe kutoka kwenye kifungo hicho siku ya Sabato?” Aliposema mambo hayo, wapinzani wake wote wakaanza kuaibika, lakini umati wote ukaanza kushangilia ulipoona mambo yenye utukufu aliyofanya » (Luka 13:10-17).
Yesu Kristo anamponya binti wa mwanamke wa Foinike: « Yesu akatoka hapo na kwenda katika eneo la Tiro na Sidoni. Na tazama! mwanamke fulani Mfoinike kutoka eneo hilo akamjia, akapaza sauti: “Nihurumie, Bwana, Mwana wa Daudi. Binti yangu anasumbuliwa kikatili na roho mwovu.” Lakini Yesu hakumjibu mwanamke huyo. Kwa hiyo wanafunzi wake wakaja na kumwambia: “Mwambie aende, kwa sababu anaendelea kutufuata akipaza sauti.” Yesu akajibu: “Sikutumwa kwa yeyote isipokuwa kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli.” Lakini mwanamke huyo akaja na kumsujudia akisema: “Bwana, nisaidie!” Yesu akamjibu: “Haifai kuuchukua mkate wa watoto na kuwatupia mbwa wadogo.” Mwanamke huyo akasema: “Ndiyo Bwana, lakini hata hao mbwa wadogo hula makombo yanayoanguka kutoka kwenye meza ya mabwana wao.” Ndipo Yesu akamwambia: “Ewe mwanamke, imani yako ni kubwa; na itendeke kama unavyotaka.” Na kuanzia saa hiyo binti yake akapona » (Mathayo 15:21-28).
Yesu Kristo anazuia dhoruba: « Alipopanda kwenye mashua, wanafunzi wake wakamfuata. Na tazama! dhoruba kubwa ikatokea baharini, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua; lakini Yesu alikuwa amelala usingizi. Wakaja na kumwamsha wakisema: “Bwana, tuokoe, tuko karibu kuangamia!” Lakini akawauliza: “Kwa nini mnaogopa sana, ninyi wenye imani ndogo?” Kisha akasimama na kuukemea upepo na bahari, kukawa shwari kabisa. Basi wanafunzi wakashangaa na kusema: “Huyu ni mtu wa aina gani? Hata upepo na bahari vinamtii” » (Mathayo 8:23-27). Muujiza huu unaonyesha kuwa katika paradiso ya kidunia hakutakuwapo tena dhoruba au mafuriko ambayo yatasababisha misiba.
Yesu Kristo akitembea juu ya bahari: « Baada ya kuuaga umati, akapanda mlimani akiwa peke yake ili kusali. Ilipofika jioni, alikuwa peke yake huko. Kufikia sasa mashua ilikuwa mamia ya mita kutoka kwenye nchi kavu, ikitaabishwa na mawimbi kwa sababu upepo ulikuwa ukivuma kinyume chao. Lakini katika kesha la nne la usiku akawajia, akitembea juu ya bahari. Wanafunzi walipomwona akitembea juu ya bahari, wakahangaika na kusema: “Ni mzuka!” Wakapaza sauti kwa hofu. Lakini mara moja Yesu akawaambia: “Jipeni moyo! Ni mimi; msiogope.” Petro akamjibu: “Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako nikitembea juu ya maji.” Akamwambia: “Njoo!” Ndipo Petro akatoka kwenye mashua, akatembea juu ya maji kumwelekea Yesu. Lakini alipoitazama ile dhoruba ya upepo akaogopa. Alipoanza kuzama, akapaza sauti: “Bwana, niokoe!” Mara moja Yesu akaunyoosha mkono wake, akamshika na kumwambia: “Wewe mwenye imani ndogo, kwa nini umekuwa na shaka?” Walipopanda kwenye mashua, ile dhoruba ikatulia. Ndipo wale waliokuwa ndani ya mashua wakamsujudia wakisema: “Kwa kweli wewe ni Mwana wa Mungu.” » (Mathayo 14:23-33).
Uvuvi kwa kimuujiza: « Pindi moja, Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa la Genesareti na umati ulikuwa umemsonga ili kusikiliza neno la Mungu. Akaona mashua mbili zikiwa zimeegeshwa kando ya ziwa, lakini wavuvi walikuwa wametoka na walikuwa wakiosha nyavu zao. Akaingia katika mashua moja iliyokuwa ya Simoni, akamwomba aivute mbali kidogo na nchi kavu. Kisha akaketi na kuanza kuwafundisha watu akiwa kwenye mashua. Alipoacha kuzungumza, akamwambia Simoni: “Peleka mashua mahali penye kina, kisha mshushe nyavu zenu, mvue samaki.” Simoni akamjibu: “Mwalimu, tumejitahidi kuvua samaki usiku wote na hatukupata chochote, lakini nitazishusha nyavu kama ulivyoniagiza.” Basi walipofanya hivyo, wakavua samaki wengi sana hivi kwamba nyavu zao zikaanza kukatika. Wakawaita wenzao waliokuwa katika ile mashua nyingine waje kuwasaidia, wakaja na kujaza mashua zote mbili, nazo zikaanza kuzama. Simoni Petro alipoona hivyo, akaanguka magotini pa Yesu na kusema: “Bwana ondoka kwangu, kwa sababu mimi ni mtu mwenye dhambi.” Kwa maana yeye na wenzake walishangazwa sana na samaki wengi waliovua. Pia, Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo, ambao walishirikiana na Simoni wakashangaa. Lakini Yesu akamwambia Simoni: “Acha kuogopa. Kuanzia sasa utakuwa ukiwavua watu wakiwa hai.” Basi wakazirudisha mashua kwenye nchi kavu, wakaacha kila kitu na kumfuata » (Luka 5:1-11).
Yesu Kristo anazidisha mikate: « Baada ya hapo Yesu akavuka Bahari ya Galilaya, au Tiberia. Na umati mkubwa sana ulikuwa ukimfuata, kwa sababu walikuwa wakiona ishara za miujiza alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa. Basi Yesu akapanda mlimani, akaketi huko pamoja na wanafunzi wake. Sasa Pasaka, ile Sherehe ya Wayahudi, ilikuwa imekaribia. Yesu alipoinua macho yake na kuona umati mkubwa ukija, akamuuliza Filipo: “Tutanunua wapi mikate ili watu hawa wale?” Hata hivyo, aliuliza swali hilo ili kumjaribu, kwa maana alijua jambo alilokuwa karibu kufanya. Filipo akamjibu: “Mikate ya dinari 200 haiwezi kutosha hata tukimpa kila mmoja wao kipande kidogo.” Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, ndugu ya Simoni Petro, akamwambia: “Hapa kuna mvulana mdogo aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili wadogo. Je, hivi vitawatosha watu wengi hivi?” Yesu akasema: “Waambieni watu waketi.” Basi mahali hapo palikuwa na nyasi nyingi, nao watu wakaketi, karibu wanaume 5,000. Yesu akaichukua ile mikate, akatoa shukrani, kisha akawagawia wale waliokuwa wameketi hapo; pia akafanya vivyo hivyo na wale samaki wadogo, watu wote wakala na kushiba. Waliposhiba akawaambia wanafunzi wake: “Kusanyeni vipande vilivyobaki, ili chochote kisipotee.” Basi wakakusanya vipande vilivyobaki wakajaza vikapu 12 baada ya watu kula kutokana na ile mikate mitano ya shayiri. Watu walipoona muujiza aliofanya, wakaanza kusema: “Kwa kweli huyu ndiye Nabii aliyepaswa kuja ulimwenguni.” Kisha Yesu akijua walitaka kuja kumkamata wamfanye awe mfalme, akaondoka tena akaenda mlimani akiwa peke yake » (Yohana 6:1-15). Kutakuwa na chakula tele katika dunia yote (Zaburi 72:16; Isaya 30:23).
Yesu Kristo humfufua mwana wa mjane: « Muda mfupi baadaye, Yesu akasafiri pamoja na wanafunzi wake na umati mkubwa kwenda jiji linaloitwa Naini. Alipokaribia lango la jiji, tazama! kulikuwa na watu waliokuwa wamebeba maiti wakiipeleka nje, yule aliyekufa alikuwa mwana pekee, na mama yake alikuwa mjane. Watu wengi kutoka jijini walikuwa pamoja na yule mwanamke. Bwana alipomwona yule mjane akamsikitikia na kumwambia: “Acha kulia.” Akakaribia na kuligusa jeneza, nao wale waliolibeba wakasimama. Akasema: “Kijana, ninakuambia, inuka!” Yule mfu akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake. Basi wote wakaogopa, wakaanza kumtukuza Mungu wakisema: “Nabii mkuu ameinuliwa kati yetu,” na, “Mungu amewakumbuka watu wake.” Habari hizo kumhusu Yesu zikaenea katika Yudea yote na maeneo jirani » (Luka 7:11-17).
Yesu Kristo humfufua binti ya Yairo: « Alipokuwa bado akizungumza, mwakilishi wa yule ofisa msimamizi wa sinagogi akaja na kusema: “Binti yako amekufa, usiendelee kumsumbua Mwalimu.” Yesu aliposikia hilo akamwambia: “Usiogope, uwe tu na imani, naye ataokolewa.” Alipofika kwenye nyumba hiyo, hakumruhusu yeyote aingie pamoja naye ila Petro, Yohana, Yakobo, na wazazi wa yule msichana. Lakini watu wote walikuwa wakilia na kujipigapiga kwa huzuni kwa sababu ya yule msichana. Basi akawaambia: “Acheni kulia, kwa maana hajafa bali amelala usingizi.” Ndipo wakaanza kumcheka kwa dharau, kwa sababu walijua amekufa. Lakini akamshika mkono na kumwita: “Mtoto, inuka!” Roho yake ikarudi naye akasimama mara moja, kisha Yesu akaagiza apewe chakula. Basi, wazazi wake wakafurahi sana, lakini Yesu akawaagiza wasimwambie mtu yeyote kilichotukia » (Luka 8:49-56).
Yesu Kristo anamfufua rafiki yake Lazaro, ambaye alikuwa amekufa siku nne zilizopita: « Yesu hakuwa ameingia kijijini, bado alikuwa mahali alipokutana na Martha. Wayahudi waliokuwa pamoja na Maria nyumbani wakimfariji, walipomwona akisimama upesi na kuondoka, wakamfuata wakidhani kwamba alikuwa akienda kulia kwenye kaburi. Maria alipofika mahali alipokuwa Yesu na kumwona, akaanguka miguuni pake na kumwambia: “Bwana, kama ungekuwa hapa, ndugu yangu hangekufa.” Yesu alipomwona akilia na Wayahudi waliokuja pamoja naye wakilia pia, akaugua moyoni na kutaabika. Akauliza: “Mmemlaza wapi?” Wakamjibu: “Bwana, njoo uone.” Yesu akatokwa na machozi. Ndipo Wayahudi wakaanza kusema: “Ona jinsi alivyompenda!” Lakini baadhi yao wakauliza: “Je, mtu huyu aliyemfungua macho yule kipofu hangeweza kuzuia huyu asife?”
Kisha baada ya Yesu kuugua tena moyoni, akaja kwenye lile kaburi. Kwa kweli, lilikuwa pango lililofunikwa kwa jiwe. Yesu akasema: “Liondoeni jiwe.” Martha, dada ya yule aliyekufa akamwambia: “Bwana, kufikia sasa lazima awe ananuka, kwa maana ni siku nne.” Yesu akamwambia: “Je, sikukuambia kwamba ukiamini utauona utukufu wa Mungu?” Basi wakaliondoa lile jiwe. Kisha Yesu akatazama mbinguni na kusema: “Baba, ninakushukuru kwa sababu umenisikia. Kwa kweli, ninajua kwamba sikuzote wewe hunisikia; lakini nilisema kwa ajili ya umati waliosimama kunizunguka, ili waamini kwamba ulinituma.” Baada ya kusema hayo, akaita kwa sauti kubwa: “Lazaro, njoo huku nje!” Mtu huyo aliyekuwa amekufa akatoka, miguu na mikono yake ikiwa imefungwa kwa vitambaa, na uso wake ukiwa umefungwa kwa kitambaa. Yesu akawaambia: “Mfungueni, mmwache aende »” (Yohana 11:30-44).
Uvuvi wa mwisho wa kimuujiza (muda mfupi baada ya ufufuo wa Kristo): « Hata hivyo, kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya bahari, lakini wanafunzi hawakutambua ni Yesu. Basi Yesu akawauliza: “Watoto, mna chakula chochote?” Wakamjibu: “Hapana!” Akawaambia: “Utupeni wavu upande wa kulia wa mashua, nanyi mtapata.” Basi wakautupa, lakini wakashindwa kuuvuta kwa sababu samaki walikuwa wengi sana. Ndipo mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro: “Ni Bwana! Simoni Petro, aliposikia kwamba ni Bwana, akavaa vazi lake la nje kwa maana alikuwa uchi, akajitumbukiza baharini. Lakini wale wanafunzi wengine wakaja katika ile mashua ndogo, wakiukokota wavu wenye samaki wengi kwa maana hawakuwa mbali na nchi kavu, walikuwa umbali wa mita 90 hivi » (Yohana 21:4-8).
Yesu Kristo alifanya miujiza mingine mingi. Wao huimarisha imani yetu, wanatutia moyo na wanapata baraka nyingi ambazo zitakuwa duniani. Maneno yaliyoandikwa ya mtume Yohana yanahitimisha vizuri idadi kubwa ya miujiza ambayo Yesu Kristo alifanya, kama dhamana ya kitakachotokea duniani: « Kwa kweli, pia kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa kirefu, nadhani ulimwengu haungekuwa na nafasi ya kuviweka vitabu vya kukunjwa ambavyo vingeandikwa » (Yohana 21:25).
***
Makala Nyingine za Kujifunza Biblia:
Neno lako ni taa ya miguu yangu na mwanga wa njia yangu (Zaburi 119:105)
Sherehe ya ukumbusho wa kifo cha Yesu Kristo
Kwa nini Mungu aliruhusu kuteseka na uovu?
Mafundisho ya msingi ya Biblia
Nini cha kufanya kabla ya dhiki kuu?
Other African languages:
Afrikaans: Ses Bybelstudie-artikels
Amharic: ስድስት የመጽሐፍ ቅዱስ ጥናት ርዕሶች
Haussa: Labarun nazarin Littafi Mai Tsarki guda shida
Igbo: Akụkọ isii gbasara Akwụkwọ Nsọ
Malagasy: Lohahevitra Fianarana Baiboly Enina
Somali: Lix Mawduuc oo Barashada Kitaabka Quduuska ah
Xhosa: Amanqaku Aza Kufundwa IBhayibhile Amathandathu
Yoruba: Àkòrí mẹ́fà ti Ìkẹ́kọ̀ọ́ Bíbélì
Zulu: Izindikimba Eziyisithupha Zokufunda Ibhayibheli
Arabic: ستة مواضيع لدراسة الكتاب المقدس
Menyu ya muhtasari katika lugha zaidi ya 70, kila moja ikiwa na makala sita muhimu za Biblia…
Table of contents of the http://yomelyah.fr/ website
Soma Biblia kila siku. Maudhui haya yanajumuisha makala za Biblia za kuelimisha katika Kiingereza, Kifaransa, Kihispania na Kireno (ukitumia Google Tafsiri, chagua lugha na lugha unayopendelea ili kuelewa maudhui)…
***